Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amehutubia waalimu, majaji na wasomi wa Qur'ani Tukufu walioshiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya 27 ya Qur'ani Tukufu katika katika hadhara iliyokusanyika kwenye Husainiya ya Imam Khomeini sambamba na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam Hussain (as). Ayatullah Khamenei ameitaja Qur'ani kuwa ni kamba madhubuti ya Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa Qur'ani imeahidi maisha bora ambayo ni yale yanayoambatana na heshima, amani, hali bora ya kimaisha, uhuru, elimu, maendeleo, maadili mema, upole na usamehevu; mambo ambayo yanawezekana kwa kuanisika na Qur'ani na kushikamana na kamba hiyo ya Mwenyezi Mungu.
Mwanzoni mwa mahfali hiyo washindi wa mashindano ya kimataifa ya kusoma na kuhifadhi Qur'ani walitia nuru majlisi hiyo kwa visomo vya kitabu hicho kitakatifu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kuanisika na Qur'ani hutayarisha uwanja wa maarifa ya kitabu hicho kupenya na kuingia katika roho na nyoyo za Waislamu. Ameongeza kuwa kwa miaka mingi sasa kunafanyika jitihada kubwa za kutenganisha baina ya maarifa ya Qur'ani na nyoyo za umma wa Kiislamu kwa kadiri kwamba katika baadhi ya nchi za Kiislamu somo la jihadi limefutwa mashuleni kwa ajili ya kuwaridhisha maadui wa Uislamu.
Akifafanua maisha bora yaliyoahidiwa na Qur'ani Tukufu, Ayatullah Khamenei amesema: "Katika maisha hayo bora kuna maisha ya mtu binafsi na ya kijamii, roho na mwili wa mwanadamu na dunia na akhera."
Amesema katika maisha bora ya Qur'ani kumedhaminiwa utulivu wa kiroho, amani, saada na ufanisi, heshima ya kijamii, kujitawala na uhuru kwa watu wote. Amesisitiza kuwa sharti la kupata maisha ya aina hiyo ni kufanya vikao na mashindano ya Qur'ani na kulea watu waliohifadhi Qur'ani na makarii wa kitabu hicho.
Amewausia pia vijana kutaamali na kukifahamu vyema kitabu kitukufu cha Qur'ani na kuhifadhi aya zake na kuongeza kuwa kila mara mwanadamu anapokaa na kusimama na Qur'ani huondokewa na pazia ya ujinga na kufunguliwa mto wa nuru na mwanga.
Vilevile Ayatullah Khamenei amehimiza kuwahamasisha watoto na mabarobaro suala la kuhifadhi Qur'ani na kusema kuwa kuhifadhi Qur'ani humpa mtu fursa ya kutaamali katika aya za kitabu hicho kutokana na kukariri aya hizo. Amesema tunapaswa kuthamini neema ya kuhifadhi Qur'ani ma tusiache neema hiyo ya Mwenyezi Mungu itutoke.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuna udharura wa kusoma Qur'ani kuanzia mwanzo hadi mwisho wake kwa ajili ya kuelewa vyema maarifa na maana ya kitabu hicho na kuongeza kuwa walimu wa tafsiri wanapaswa kuweka wazi maana ya ndani ya aya za kitabu hicho na kuondoa vizuizi vya kuelewa maarifa yake.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amefanya ulinganisho wa harakati ya Qur'ani hapa nchini kabla na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na akasema: "Harakati hii adhimu imetokea katika kipindi cha miaka 31 ya hivi karibuni na vijana wengi wenye ari na hamu kubwa wamejiunga na vikao vya watu wanaohifadhi, kosoma na kutabahari ndani ya kitabu hicho."
Ayatullah Khamenei amesema kuwa taifa la Iran limekuwa na taathira kubwa ulimwenguni kutokana na kutilia maanani kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu na linasimama mkabala wa maadui likijihisi kuwa na nguvu na uwezo.
Mwanzoni mwa kikao hicho mwakilishi wa Faqihi Mtawala ambaye pia ni Mkuu wa Jumuiya ya Wakfu ya Mambo ya Kheri ya Iran Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadi ametoa ripoti kuhusu Mashindano ya 27 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yaliyomalizika jana mjini Tehran na akasema kuwa makarii na mahafidhi 95 wa Qur'ani kutoka nchi 60 duniani wameshiriki katika mashindano hayo. Ameongeza kuwa majaji 14 wa kimataifa na wa Iran pia walisimamia mashindano hayo.
Vilevile jaji wa mashindano hayo kutoka Misri Dakta Farajullah Shadhili alisoma aya kadhaa za Qur'ani na kuzungumzia minasaba ya kubaathiwa Mtume Muhammad (saw) na kuzaliwa mjukuu wake Imam Hussein (sa). Dakta Shadhili ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuipa umuhimu Qur'ani Tukufu.