Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amekutana na viongozi wa ofisi za Faqihi Mtawala katika vyuo vikuu na kusema kuwa hali inayotawala sasa katika vyuo vikuu inaridhisha kikamilifu katika pande kadhaa. Ayatullah Khamenei amesema maendeleo na harakati za kielimu za vyuo vikuu, kambi za jihadi zisizokuwa na kifani za wanachuo, mwamko na maarifa yao ya kisiasa, kuwapo kwao katika medani mbalimbali muhimu, anga ya kidini inayotawala kati ya wanafunzi wa vyuo vikuu na idadi kubwa ya wahadhiri wenye imani na wanaojali mustakbali wa nchi yao ni uhakika unaong'ara katika mazingira ya vyuo vikuu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kuwapo kwa wanazuoni bora katika vyuo vikuu na mawasiliano yao mazuri na ya karibu na wanafunzi na wahadhiri ni miongoni mwa neema kubwa za Mwenyezi Mungu za baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa fursa hii muhimu mno na yenye thamani inapaswa kutumiwa vyema, na umuhimu wake unaweza kushuhudiwa vizuri zaidi katika propaganda chafu na wasiwasi unaodhihirishwa na wasioitakia nchi hii kheri kuhusu mpango wa kuvifanya vyuo vikuu kuwa vya Kiislamu; kwani moja ya madhihirisho ya vyuo vikuu vya Kiislamu ni kuwapo wanazuoni wa kidini katika vyuo hivyo.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia hali ya vyuo vikuu hapa nchini na akasema inasikitisha kuona kuna baadhi ya watu wanaosisitiza tu juu ya nukta hasi na kuzikuza kupindukia, na wakati kunapozungumziwa hali ya kuridhisha kuhusu mazingira ya vyuo vikuu na vijana, watu hao hufasiri hilo kuwa ni alama ya kutoelewa hali halisi ilivyo katika vyuo hivyo.
Ameongeza kuwa, kusifu hali ya vyuo vikuu hakuna maana ya kufumbia macho baadhi ya nukta hasi na kwamba mambo yote yanapaswa kutazamwa kwa pamoja ili tuweze kufikia kwenye natija nzuri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia ripoti iliyotolewa na Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadiyan, Mkuu wa Chombo cha Wawakilishi wa Fakihi Mtawala katika Vyuo Vikuu vya Iran na kusisitiza kwamba kwa kuzingitia propaganda mbaya na kubwa zinazofanywa na maadui na uhakika wa kielimu na kidini unaotawala katika vyuo vikuu, tunaweza kusema bila ya kusita kuwa mazingira ya vyuo hivyo hivi sasa ni bora na ya kuridhisha.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, kwa kuchunguza hali ya vyuo vikuu si sawa kutarajia kuona hali iliyopo katika vyuo vya kidini ikitawala mazingira ya wanafunzi wa vyuo vikuu.
Amesisitizia pia juu ya udharura wa kuzingatiwa kwa wakati mmoja masuala ya kiitikadi na kiroho ya wanachuo na kuongeza kuwa, misingi ya kifikra ya wanachuo inapaswa kuimarishwa kwa namna ambayo si tu wanafunzi wa vyuo vikuu hawataathirika na mambo hasi lakini pia wawe na uwezo wa kuathiri mazingira yao na kuwa na uwezo mkubwa wa Kifikra.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kutilia maanani masuala ya kimaanawi na kiroho ya wanafunzi wa vyuo vikuu ndio msingi na nguzo yao ya kiitikadi. Amesisitiza kuwa, nyoyo za vijana zinapaswa kuelekezwa kwenye dhikri, unyenyekevu na kumjua Mwenyezi Mungu kwa kutumia nasaha, mawaida mema na mwenendo mzuri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa, miongoni mwa masharti ya kuzifanya nyoyo za vijana ziathirike ni nasaha za kirafiki sambamba na amali njema na ikhasi katika matendo. Amesisitiza juu ya udharura wa kutolewa darsa za maarifa ya Kiislamu kwa kutumia lugha ya kisasa na inayooana na fikra na fasihi wanachuo. Ameongeza kuwa, Hawza na vyo vikuu vya kidini vina majukumu mazito sana katika kuzisaidia kielimu na kwa nguvu kazi ofisi za wawakilishi wa Fakihi Mtawala katika vyuo vikuu nchini.
Vilevile Ayatullah Khamenei amesema kuwa, taasisi za serikali pia zina jukumu zito sana katika suala hilo. Amesisitiza kuwa, tofauti na huko nyuma, kwa bahati nzuri serikali ya sasa imeandaa mazingira mazuri zaidi ya kushiriki wanazuoni wa kidini katika vyuo vikuu na kwamba neema hiyo inapaswa kushukuriwa kwa kutumia vyema fursa hiyo.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadiyan, Mkuu wa Chombo cha Wawakilishi wa Fakihi Mtawala katika Vyuo Vikuu vya Iran ametoa ripoti fupi ya kazi za chombo hicho na kusema kuwa miongoni mwa kazi hizo ni kufanyika ibada za itikafu katika vyuo vikuu, sala za jamaa, vikao na kaambi za jihadi ya wanachuo na kujitokeza kwa wingi mno vijana wanachuo kwa ajili ya kwenda kwenye amali ya umra.